Numbers 35:9-34

9Kisha Bwana akamwambia Mose: 10 a“Sema na Waisraeli, uwaambie: ‘Mtakapovuka Yordani kuingia Kanaani, 11 bchagueni baadhi ya miji iwe miji yenu ya makimbilio, ambayo mtu ambaye ameua mwenzake bila kukusudia aweza kukimbilia humo. 12 cItakuwa mahali pa kukimbilia kutoka mlipiza kisasi, ili kwamba mtu aliyeshtakiwa kwa mauaji asife kabla ya kujitetea mbele ya mkutano. 13Miji hii sita mtakayoitoa itakuwa miji yenu ya makimbilio. 14 dMtatoa miji mitatu ngʼambo hii ya Yordani na miji mingine mitatu upande wa Kanaani kama miji ya makimbilio. 15 eMiji hii sita itakuwa mahali pa makimbilio kwa ajili ya Waisraeli, wageni na watu wengine wanaoishi katikati yenu, ili kwamba mtu yeyote ambaye ameua mtu mwingine pasipo kukusudia aweze kukimbilia humo.

16 f“ ‘Kama mtu akimpiga mwenzake kwa chuma naye mtu huyo akafa, mtu huyo ni muuaji; muuaji sharti atauawa. 17Au kama mtu analo jiwe mkononi mwake ambalo laweza kuua, naye akampiga mwenzake akafa, yeye ni muuaji; muuaji huyo sharti atauawa. 18Au kama mtu ana chombo cha mti mkononi mwake ambacho chaweza kuua, naye akampiga mwenzake akafa, yeye ni muuaji; muuaji huyo sharti atauawa. 19Mlipiza kisasi cha damu atamuua muuaji; wakati akikutana naye, atamuua. 20 gIkiwa mtu ana chuki ya siku nyingi na mwenzake akamsukuma au akamtupia kitu kwa kukusudia naye akafa, 21 hau ikiwa katika uadui akampiga ngumi naye akafa, mtu yule sharti atauawa; yeye ni muuaji. Mlipiza kisasi cha damu atamuua muuaji atakapokutana naye.

22 i“ ‘Lakini kama mtu akimsukuma mwenziwe ghafula pasipo chuki, au kumtupia kitu pasipo kukusudia, 23au, pasipo kumwona, akimwangushia jiwe ambalo laweza kumuua naye akafa, basi kwa kuwa hakuwa adui yake naye hakukusudia kumuumiza, 24 jkusanyiko lazima liamue kati yake na mlipiza kisasi wa damu kufuatana na sheria hizi. 25 kKusanyiko ni lazima limlinde yule anayeshtakiwa kuua kutoka kwa mlipiza kisasi wa damu, na kumrudisha katika mji wa makimbilio alikokuwa amekimbilia. Lazima akae humo mpaka atakapokufa kuhani mkuu ambaye alikuwa amepakwa mafuta matakatifu.

26“ ‘Lakini kama mshtakiwa atatoka nje ya mipaka ya mji wa makimbilio ambao amekimbilia, 27 lna mlipiza kisasi wa damu akamkuta nje ya mji, mlipiza kisasi wa damu anaweza kumuua mshtakiwa huyo bila kuwa na hatia ya kuua. 28Mshtakiwa lazima akae katika mji wake wa makimbilio mpaka atakapokufa kuhani mkuu; atarudi tu kwenye mali yake baada ya kifo cha kuhani mkuu.

29 m“ ‘Hizi ndizo kanuni za sheria zitakazohitajiwa kwenu na katika vizazi vyenu vijavyo, popote mtakapoishi.

30 n“ ‘Yeyote anayeua mtu atauawa kama muuaji ikiwa tu kuna ushuhuda wa mashahidi. Lakini hakuna mtu atakayeuawa kwa ushuhuda wa shahidi mmoja tu.

31 o“ ‘Usikubali fidia yoyote ya kuokoa uhai wa muuaji ambaye anastahili kufa. Mtu huyo hakika lazima auawe.

32 p“ ‘Usikubali fidia ya mtu yeyote ambaye amekimbilia katika mji wa makimbilio na kumruhusu kurudi kuishi katika nchi yake kabla ya kifo cha kuhani mkuu.

33 q“ ‘Msiinajisi nchi mnayoishi. Umwagaji damu hunajisi nchi, na upatanisho hauwezekani kufanyika katika nchi ambayo damu imemwagwa, isipokuwa tu kwa damu ya yule aliyeimwaga damu. 34 rMsiinajisi nchi mnayoishi, ambayo nami ninakaa, kwa kuwa Mimi, Bwana, ninakaa katikati ya Waisraeli.’ ”

Copyright information for SwhNEN